24. Mamlaka ya Yesu Juu ya Mapepo

Written on 04/08/2024
Gordon Decker

24. Mamlaka ya Yesu Juu ya Mapepo

Jumuika:

  • Je, una nini cha kukufanya ushukuru leo?
  • Je, katika juma hili umemwona Mungu akitenda kazi kwa namna gani katika maisha yako?
  • Je, ni changamoto gani unakabiliana nazo katika maisha? Tunaweza kukusaidia vipi?
  • Je, somo la ugunduzi lililopita ulilitumiaje? Ni mambo gani yalitokea?
  • Je, ni akina nani uliwashirikisha kuhusu ugunduzi wa kipindi kilichopita? Waliitikiaje?

Maelekezo:

Tafadhali tumia hatua zifuatazo kukuongoza katika ugunduzi wa kweli ya Mungu katika kifungu cha Maandiko hapo chini.

Je, ninahitaji  kupitia Mwongozo wa Kikundi?

Gundua

Hatua ya 1: Washiriki wasome sehemu fungu la Maandiko kwa zamu (fafanua maneno mapya/msamiati)

Hatua ya 2: Mtu mmoja asome fungu zima kwa sauti wakati wengine wakisikiliza

Hatua ya 3: Mshiriki mmoja aelezee kifungu kinavyosema kwa maneno yake mwenyewe (wengine waongezee mawazo yao)

 

Mamlaka ya Yesu Juu ya Mapepo (Marko 5:1-20)

1 Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; 4kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. 6Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. 8Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. 9Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. 10Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. 11Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. 12Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. 13Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. 14Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea. 15Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. 16Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. 17Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. 18Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; 19lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. 20Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.

[Swahili Union Version (SUV): © -1952, 1997: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.]

Uliza/Jibu:

  • Je, unaona nini katika fungu hili?
  • Je, inamaanisha nini kwako?
  • Je, ni kitu gani kimekuvutia /Je ni kitu gani hujakipenda kuhusu fungu hili?
  • Je, ni kwa namna gani fungu hili limebadili namna unavyomwona Mungu/Watu?

Itikia: kama hii ni kweli…

  • Je, ni kwa namna gani Neno linaweza kubadili jinsi unavyoishi?
  • Je utamshirikisha nani kuhusu ugunduzi huu wa leo?