19. Mwokozi Azaliwa

Written on 04/13/2024
Gordon Decker

19. Mwokozi Azaliwa

Jumuika:

  • Je, una nini cha kukufanya ushukuru leo?
  • Je, katika juma hili umemwona Mungu akitenda kazi kwa namna gani katika maisha yako?
  • Je, ni changamoto gani unakabiliana nazo katika maisha? Tunaweza kukusaidia vipi?
  • Je, somo la ugunduzi lililopita ulilitumiaje? Ni mambo gani yalitokea?
  • Je, ni akina nani uliwashirikisha kuhusu ugunduzi wa kipindi kilichopita? Waliitikiaje?

Maelekezo:

Tafadhali tumia hatua zifuatazo kukuongoza katika ugunduzi wa kweli ya Mungu katika kifungu cha Maandiko hapo chini.

Je, ninahitaji  kupitia Mwongozo wa Kikundi?

Gundua

Hatua ya 1: Washiriki wasome sehemu fungu la Maandiko kwa zamu (fafanua maneno mapya/msamiati)

Hatua ya 2: Mtu mmoja asome fungu zima kwa sauti wakati wengine wakisikiliza

Hatua ya 3: Mshiriki mmoja aelezee kifungu kinavyosema kwa maneno yake mwenyewe (wengine waongezee mawazo yao)

 

Mwokozi Azaliwa (Luka 2:1-20)

1 Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. 2 Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. 3 Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. 4 Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; 5 ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. 6 Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, 7 akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. 8 Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. 10 Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11 maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe. 13 Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, 14 Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. 15 Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. 16 Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. 17 Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 18 Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 19 Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 20 Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.

[Swahili Union Version (SUV): © -1952, 1997: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.]

Uliza/Jibu:

  • Je, unaona nini katika fungu hili?
  • Je, inamaanisha nini kwako?
  • Je, ni kitu gani kimekuvutia /Je ni kitu gani hujakipenda kuhusu fungu hili?
  • Je, ni kwa namna gani fungu hili limebadili namna unavyomwona Mungu/Watu?

Itikia: kama hii ni kweli…

  • Je, ni kwa namna gani Neno linaweza kubadili jinsi unavyoishi?
  • Je utamshirikisha nani kuhusu ugunduzi huu wa leo?