Mfumo wa M28 (Model)

Written on 05/10/2024
Gordon Decker


M28 ni nini?

Rahisi. Mahsusi. Endelevu

Mpango wa kuwafanya Mataifa yote kuwa Wanafunzi wa Yesu uitwao M28 (ikiwakilisha Mathayo 20:18-20) ni mkakati rahisi, mahsusI, na endelevu ambao umeandaliwa kwa ajili ya watu ya watu wenye mahitaji ya kiroho, kuwawezesha kuifahamu kweli, kuwaongoza kuwa na uhusiano binafsi na Yesu (kumpokea kama Bwana na Mwokozi wao), na kuwandaa kwa ajili ya kuwafanya wengine kuwa wanafunzi wa Yesu popote walipo. Mpango huu unawasaidia watu kuwa sehemu ya jamii halisi ya Kibiblia huku ukiwapa nafasi ya kujifunza kweli ya Mungu inayoweza kubadilisha maisha yao binafsi.

M28 ni mtindo wa maisha, siyo utaratibu wa kimazoea tu. Watu wanaotumia mchakato wa M28 hanza kupokea vinasaba vya uzidisho wa kiroho kuanzia katika siku ya kwanza ya kuutumia mpango huu. M28 hutenda kazi katika mazingira ya utamaduni na ngazi yoyote ya jamii.


Maono ya M28

Kubadilisha mataifa kwa kuzalisha jamii zinazowafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu katika ngazi yoyote ya jamii.


Tunu za M28

  • Ongoza kama mtumishi
  • Anza kidogo ili kukua haraka
  • Mafanikio ni utii
  • Wezesha, usifundishe
  • Wafanye kuwa wanafunzi ili kuwaongoza kwa Yesu
  • Andaa watu wa kuwafanya wengine kuwa wanafunzi wa Yesu
  • Mahusiano mazuri huleta matokeo makubwa zaidi
  • Uwe tayari kwa usiyoyatarajia
  • Tarajia miujiza

[Zimenukuliwa kutoka kwa David Watson. Zimetumika kwa ruhusa ya Wachapishaji]

​Mathayo 28:18-20

18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; 20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Swahili Union Version (SUV): @1952, 1997: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.


Jinsi M28 inavyotumika

​Unachohitaji ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu kuwaongoza watu kwenye Kweli, na kama wataamua kuitii, mabadiliko yatatokea!

Msingi wa Mpango wa M28 wa kuwafanya Mataifa yote kuwa wanafunzi ni uzoefu wa Uvumbuzi wa Kibiblia wa M28.

Mara  mtu mwenye mahitaji ya kiroho anapobainishwa, tunakutana nao ili kupitia mchakato huu rahisi wa uvumbuzi wa kweli pamoja nao. Baadaye, wanatiwa moyo kufanya hivyo na rafiki zao, familia, au watu wengine wanaowafahamu ili kuwashirikisha kilichotokea. Huo ndio mwanzo wa Uvumbuzi wa Kibiblia wa M28.

 Uvumbuzi wa Kibiblia wa M28 unajikita kwenye Neno la Mungu ambalo ndiyo mamlaka ya mwisho kwa ajili maisha yetu na mwenendo, na Roho Mtakatifu kama Kiongozi wetu Mkuu. Kwa kusimamia kwenye fungu moja la Biblia kwa wakati mmoja, bila kutumia vyanzo vingine vya nje ya hapo, tunawaalika wote walio kwenye Kikundi kushiriki katika uvumbuzi wa kweli inayofundishwa na kuiweka kwenye vitendo (kama Mwongozo wa Mwezeshaji wa M28 unavyoelekeza). Maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa Uvumbuzi wa Biblia wa M28 ni Kujiunga (katika Ushirika na wengine), Kugundua (kweli ya Mungu), na Kuitikia (kile walichojifunza).

Uvumbuzi wa Biblia wa M28 – Vifungu Muhimu


Maelekezo
Kwa kila kipindi cha uvumbuzi, unahitaji kujikita kwenye kifungu kimoja cha Biblia ili kugundua mambo ambayo Mungu anataka kila mshiriki ayaone, ayaelewe, ayatii, na kuwashirikisha wengine. Kama unapitia katika mpango huu kwa mara ya kwanza, tafuta Mkufunzi wa M28 anayeweza kukusaidia. Kwa kuwa tunaweza tusipate muda wa miaka miwili wa kukutana kila juma na kundi lilelile, orodha ya “Simulizi ya Mungu” imeandaliwa kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kupata picha kamili kwa upana na kukutana na Mungu wa Biblia ndani ya muhula mmoja wa masomo (utahitaji kuchagua idadi ya vifungu vinavyolingana na ratiba ya muhula mmoja wa masomo).

Viongozi wa Vikundi/Wakufunzi
Mnaweza kuongeza au kuruka baadhi ya vifungu kama itahitajika, kulingana na mahitaji au mambo yanayojitokeza wakati wa kipindi cha majadiliano (au kutoka kwa Mwezeshaji). Kwa mfano, kama baadhi ya wanafunzi wanakabiliana na changamoto za hofu, mnaweza kufanya Uvumbuzi wa Biblia kutoka Zaburi ya 143.

Muhimu:
Siku zote wape wanafunzi nafasi wao wenyewe kugundua mambo ambayo Biblia, na Mungu anasema nao kuhusu kifungu au mada husika.

Uvumbuzi wa mambo ya Kibiblia wa M28 – Muda
Kipindi kimoja cha kujifunza na kugundua mambo ya Kibiblia cha M28 kinaweza kuchukua muda wa   saa nzima,   japo ukiweza kutumia saa moja na nusu hadi masaa mawili ni bora zaidi (kama muda unaruhusu) ili kutoa nafasi kwa ajili ya watu kushirikiana zaidi na kujadiliana kwa kina vifungu vya Biblia. Njia nzuri ya kugawanya muda kwa ajili ya maeneo ya msingi ya kikundi cha M28 ni kama ifuatavyo: Muda wa kujumuika ili kuimarisha Ushirika 25%, Ugunduzi 50%, na Mwitikio 25%.

​Uvumbuzi wa Biblia wa M28– Maandalizi
Hatua ya Kwanza – Mkufunzi wa M28 atamwomba mshiriki wa kikundi kuongoza kipindi cha juma linalofuata.

Hatua ya Pili – Mkufunzi wa M28 atakutana na mwongoza Kikundi aliyemteua kabla ya kipindi cha Uvumbuzi wa Biblia wa M28 ili kupitia Mwongozo wa Mwezeshaji na mchakato wa uwezeshaji, kujibu maswali, na kufanya maombi.

Hatua ya Tatu – Mkufunzi wa M28 ataomba kila siku kwa ajili ya kipindi kijacho cha Uvumbuzi wa Biblia wa M28 na pia atakuwa anakiombea kipindi wakati kikiwa kinaendelea.
 ​

Uvumbuzi Biblia wa M28 – Uwezeshaji

Hatua ya Kwanza – Mwezeshaji atafungua kipindi kwa kumkaribisha kila mmoja kwenye kipindi cha uvumbuzi cha siku hiyo.

Hatua ya Pili – Mwezeshaji atasoma Mwongozo wa Kikundi kwa sauti kwa ajili ya kundi zima (atarudia kufanya hivi kila baada ya majuma kadhaa, na pale unapohisi kundi linapoteza mwelekeo).

Hatua ya Tatu – Mwezeshaji atakiongoza kikundi kwa kutumia Maswali ya Mwongozo wa Mwezeshaji na kumhamasisha kila aliyehudhuria kushiriki kikamilifu.

Hatua ya Nne – Mwezeshaji atahitimisha mjadala kwa maombi au kutoa nafasi kwa mshiriki atakayejitolea kuomba.

Hatua ya Tano – Kikundi kitaamua juu ya siku ya kukutana tena na mahali watakapokutana.

Ugunduzi wa Biblia wa M28 – Ufuatiliaji

Kutana na Mwezeshaji wa kipindi kilichopita ili kumshukuru na kumtia moyo, pata mrejesho juu ya mambo waliyojifunza, jibu maswali yoyote yatayojitokeza, kisha mwombee.


Simulizi za M28

Mfumo wa M28 wa kuwafanya watu kuwa Wanafunzi wa Yesu umethibitishwa kuwa na ufanisi mkubwa baada ya kujaribiwa katika mataifa mbalimbali kama vile Australia, China, India, Japani, Nepal, katika mataifa kadhaa ya Afrika, Ujerumani, Ufilipino, na Marekani. Maelfu ya watu wamefundishwa kwa kutumia njia hii ya mfumo wa kufanya wanafunzi wa M28. Mpango huu wa aina ya kipekee unaendelea kupenya katika makundi mbalimbali ya kijamii kwa njia ya kuzidisha vikundi vya wafuasi wa Yesu Kristo ambavyo vimekua vikifikia jamii zao kwa ufanisi mkubwa, kufanya watu kumjua Mungu na Ukweli, na kuwajengea uwezo wa kuwa wanafunzi wanaowandaa wengine kuwa wanafunzi wa Yesu.
 
Mungu anaendelea kutenda mambo ya kustaajabisha duniani kote leo! Simulizi zifuatazo za M28 zimewekwa kwa ajili ya kutangaza sifa za kazi yake ya ukombozi na kukutia moyo wewe unapoendelea  kugundua na kuongeza juhudi zako  katika huduma ya M28. Simulizi hizi ni za kweli (siyo za kubuni), ingawa majina ya wahusika na  mahali walipo yamebadilishwa kwa ajili ya usalama   wa wanaoishi katika mazingira hatarishi Ulimwenguni. Ni maombi na matumaini yetu kuwa Mungu atakuzidishia kile ulichowekeza katika huduma yako ya M28 --- na kupitia mabadiliko ya milele ya maisha ya watu ndani na nje ya nchi yako.

Ni matatizo ya kifamilia huko kwao Indonesia yaliyomfanya Farah kutafuta faraja na msaada. Alishiriki katika kipindi cha Ugunduzi Biblia cha M28 kupitia mwaliko wa rafiki yake, Mungu akaanza kufanya kazi ndani ya moyo wake. Alipofanya sala ya kumpokea Kristo, alishuhudia jinsi alivyojisikia huru: “Hasira yote niliyokuwa nayo ndani yangu iliondoka na sasa najisikia nipo huru.”
 
Li alihudhuria kwenye kipindi cha Ugunduzi wa Biblia cha M28 chuoni kwao ambapo pia Mwislamu na Mhindu walikuwepo. Kila mmoja alipiga hatua kiroho katika kuuelewa Ukristo, ila Li aliamua kumpokea Kristo na sasa… anashiriki kwenye mafunzo ya kuanzisha Kikundi cha Ugunduzi wa Biblia cha M28 kazini kwake.

Tao alimpokea Kristo kupitia kwenye Kikundi cha Ugunduzi wa Biblia cha M28, akabatizwa, na hatimaye akarejea kwao. Akiwa anaendelea na Uanafunzi wa Yesu kwa njia ya mtandao wa Skype, alimkaribisha mwenzake aitwaye Bo kwenye Mpango wa M28 kwa naye akaanza kujifunza Neno la Mungu. Matokeo yake Bo naye akaamua kumfuata Yesu na akabatizwa.

“Bwana asifiwe kwa kutupatia nyenzo kipekee ya Mpango wa M28!  Imekuwa kama ufunguo unaotusaidia kufungua milango kwa ajili ya wengine kuendelea kueneza hazina za Neno la Mungu!!” (Taipei, Taiwan).
 
“Wanafunzi wanapojifunza na kugundua wao wenye juu ya kweli ya Neno la Mungu ni bora zaidi kuliko kuambiwa. Hii ni moja ya njia ambazo Mpango wa M28 unatumia katika kubadilisha fikra zetu.” (Mchungaji wa Marekani).
 
“Nimekuwa nikitumia… M28 katika kikundi cha Uanafunzi kwa ajili ya Vijana wenye changamoto za kitabia kwa karibia mwezi mmoja sasa. Vijana wenye tabia hizo walikua wakijihusisha na magenge uhalifu, vibarua, na ukahaba. Biblia imejidhihirisha kwao, na Roho Mtakatifu anaendelea kubadilisha maisha yao kadri wanavyoendelea kuwa karibu na Mungu kwa kulisoma Neno lake.” (Austin, Texas – Marekani).

“Ninashangazwa na jinsi Roho wa Mungu anavyoongoza vipindi hivi vya Ugunduzi wa Biblia na jinsi wanafunzi wanavyouliza maswali kwa umakini na usikivu walio nao wanaposoma Maandiko kwa mara ya kwanza. Hii ni fursa ya kipekee kusafiri pamoja na watu walio na kiu ya kiroho kwa ajili ya Ukweli ulio Hai.” (Tina – Marekani).