22. Mtu Anayemtafuta Mungu

Jumuika:

  • Je, una nini cha kukufanya ushukuru leo?
  • Je, katika juma hili umemwona Mungu akitenda kazi kwa namna gani katika maisha yako?
  • Je, ni changamoto gani unakabiliana nazo katika maisha? Tunaweza kukusaidia vipi?
  • Je, somo la ugunduzi lililopita ulilitumiaje? Ni mambo gani yalitokea?
  • Je, ni akina nani uliwashirikisha kuhusu ugunduzi wa kipindi kilichopita? Waliitikiaje?

Maelekezo:

Tafadhali tumia hatua zifuatazo kukuongoza katika ugunduzi wa kweli ya Mungu katika kifungu cha Maandiko hapo chini.

Je, ninahitaji  kupitia Mwongozo wa Kikundi?

Gundua

Hatua ya 1: Washiriki wasome sehemu fungu la Maandiko kwa zamu (fafanua maneno mapya/msamiati)

Hatua ya 2: Mtu mmoja asome fungu zima kwa sauti wakati wengine wakisikiliza

Hatua ya 3: Mshiriki mmoja aelezee kifungu kinavyosema kwa maneno yake mwenyewe (wengine waongezee mawazo yao)

 

Mtu Anayemtafuta Mungu (Yohana 3:1-21)
1 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. 2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. 3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. 4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? 5Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. 7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. 8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. 9 Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? 10 Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? 11 Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. 12 Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? 13 Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. 14 Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; 15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. 16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. 18 Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. 20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. 21 Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.

[Swahili Union Version (SUV): © -1952, 1997: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.]

Uliza/Jibu:

  • Je, unaona nini katika fungu hili?
  • Je, inamaanisha nini kwako?
  • Je, ni kitu gani kimekuvutia /Je ni kitu gani hujakipenda kuhusu fungu hili?
  • Je, ni kwa namna gani fungu hili limebadili namna unavyomwona Mungu/Watu?

Itikia: kama hii ni kweli…

  • Je, ni kwa namna gani Neno linaweza kubadili jinsi unavyoishi?
  • Je utamshirikisha nani kuhusu ugunduzi huu wa leo?