15. Imani ya Ibrahim Yajaribiwa

Jumuika:

  • Je, una nini cha kukufanya ushukuru leo?
  • Je, katika juma hili umemwona Mungu akitenda kazi kwa namna gani katika maisha yako?
  • Je, ni changamoto gani unakabiliana nazo katika maisha? Tunaweza kukusaidia vipi?
  • Je, somo la ugunduzi lililopita ulilitumiaje? Ni mambo gani yalitokea?
  • Je, ni akina nani uliwashirikisha kuhusu ugunduzi wa kipindi kilichopita? Waliitikiaje?

Maelekezo:

Tafadhali tumia hatua zifuatazo kukuongoza katika ugunduzi wa kweli ya Mungu katika kifungu cha Maandiko hapo chini.

Je, ninahitaji  kupitia Mwongozo wa Kikundi?

Gundua

Hatua ya 1: Washiriki wasome sehemu fungu la Maandiko kwa zamu (fafanua maneno mapya/msamiati)

Hatua ya 2: Mtu mmoja asome fungu zima kwa sauti wakati wengine wakisikiliza

Hatua ya 3: Mshiriki mmoja aelezee kifungu kinavyosema kwa maneno yake mwenyewe (wengine waongezee mawazo yao)

 

Imani ya Ibrahim Yajaribiwa (Mwanzo 21:1-7; 22:1-19)

Mwanzo 21:1-7

1 BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. 2 Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. 3 Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. 4 Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. 5 Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. 6 Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. 7 Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.

Mwanzo 22:1-19

1 Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. 3 Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. 4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. 5 Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. 6 Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. 7 Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? 8 Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. 9 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. 11 Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. 13 Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana. 15 Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni 16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, 17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; 18 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. 19 Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

[Swahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.]

Uliza/Jibu:

  • Je, unaona nini katika fungu hili?
  • Je, inamaanisha nini kwako?
  • Je, ni kitu gani kimekuvutia /Je ni kitu gani hujakipenda kuhusu fungu hili?
  • Je, ni kwa namna gani fungu hili limebadili namna unavyomwona Mungu/Watu?

Itikia: kama hii ni kweli…

  • Je, ni kwa namna gani Neno linaweza kubadili jinsi unavyoishi?
  • Je utamshirikisha nani kuhusu ugunduzi huu wa leo?