14. Mpango wa Mungu Kupitia Familia Moja

Jumuika:

  • Je, una nini cha kukufanya ushukuru leo?
  • Je, katika juma hili umemwona Mungu akitenda kazi kwa namna gani katika maisha yako?
  • Je, ni changamoto gani unakabiliana nazo katika maisha? Tunaweza kukusaidia vipi?
  • Je, somo la ugunduzi lililopita ulilitumiaje? Ni mambo gani yalitokea?
  • Je, ni akina nani uliwashirikisha kuhusu ugunduzi wa kipindi kilichopita? Waliitikiaje?

Maelekezo:

Tafadhali tumia hatua zifuatazo kukuongoza katika ugunduzi wa kweli ya Mungu katika kifungu cha Maandiko hapo chini.

Je, ninahitaji  kupitia Mwongozo wa Kikundi?

Gundua

Hatua ya 1: Washiriki wasome sehemu fungu la Maandiko kwa zamu (fafanua maneno mapya/msamiati)

Hatua ya 2: Mtu mmoja asome fungu zima kwa sauti wakati wengine wakisikiliza

Hatua ya 3: Mshiriki mmoja aelezee kifungu kinavyosema kwa maneno yake mwenyewe (wengine waongezee mawazo yao)

 

Mpango wa Mungu Kupitia Familia Moja (Mwanzo 12:1-8; 15:1-6; 17:1-8)

Mwanzo 12:1-8

1 BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; 2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; 3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. 4 Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. 5 Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani. 6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. 7 BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea. 8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA.

Mwanzo 15:1-6

1 Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. 2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? 3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.

4 Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. 5 Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. 6 Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.

Mwanzo 17:1-8

1 Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, 4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, 5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. 6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. 8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.

[Swahili Union Version (SUV): © -1952, 1997: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.]

Uliza/Jibu:

  • Je, unaona nini katika fungu hili?
  • Je, inamaanisha nini kwako?
  • Je, ni kitu gani kimekuvutia /Je ni kitu gani hujakipenda kuhusu fungu hili?
  • Je, ni kwa namna gani fungu hili limebadili namna unavyomwona Mungu/Watu?

Itikia: kama hii ni kweli…

  • Je, ni kwa namna gani Neno linaweza kubadili jinsi unavyoishi?
  • Je utamshirikisha nani kuhusu ugunduzi huu wa leo?